Genge la kigaidi la Jaishul-Dhulm limekiri kuhusika na shambulizi hilo la kigaidi lililotokea kwenye makao ya jeshi la polisi la Rask, kusini mashariki mwa Iran Alkhamisi jioni.
Naibu Gavana wa Sistan na Baluchistan anayehusika na msuala ya Usalama na Polisi amesema, watu 12 wameuawa shahidi katika shambulio hilo la kigaidi lililolenga makao ya jeshi la polisi huko Rask.
Kwa upande wake shirika la habari la Iran Press limeripoti kuwa, Mohammad Bagher Ghalibaf, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema, hii si mara ya kwanza kwa maadui kufanya jinai na mashambulio ya kigaidi dhidi ya usalama na ukakamavu wa Iran ya Kiislamu kwa kutumia magenge ya ukufurishaji na yanayoeneza shari. Amesema maadui hao kwa pamoja wanafanya njama za kutia doa imani thabiti ya taifa la Iran lakini wote wanapaswa kuelewa kuwa jinai zao hizo haziwezi kupita vivi hivi bila ya kupata majibu yanayostahiki.